Mchakato wa kumchagua Papa waendelea
Baada ya makadinali wa Kanisa Katoliki hapo jana kukosa kuafikiana
kuhusu ni nani atakuwa mkuu wa kanisa hilo, leo mchakato huo unaendelea
katika makao makuu ya kanisa hilo, Vatican.
Makadinali hao wanamuomba Mungu kuwa na maono ya kuweza kumchagua
kiongozi wao. Jumla ya makadinali 115 walio na jukumu la kumchagua papa
mpya baada ya Benedict wa 16 kujiuzulu mwezi uliopita, leo walihudhuria
misa ya asubuhi katika kanisa la Pauline ndani ya makao makuu ya
Vatican.
Baada ya hapo wamerejea katika kanisa dogo la Sisitine ili kupiga kura,
shughuli ambayo inatarajiwa kuwa na awamu mbili leo asubuhi na nyingine
mbili mchana wakitafuta kumchagua kiongozi wa Kanisa Katoliki
atakayekuwa na uwezo wa kukabiliana na misururu ya kashfa na mizozo ya
ndani kwa ndani inayolikumba Kanisa hilo katika miaka ya hivi karibuni.
Waumini, watalii wasubiri matokeo
Makadinali 115 wanaomchagua Papa mpya wa Katoliki
Waumini wa kanisa hilo na watalii walianza kufika katika ukumbi
wa Vatican mapema asubuhi wakitumai kushuhudia matokeo ya uchaguzi huo
na kusubiri kuuona moshi mweupe ukifuka kutoka kanisa hilo la Sisitine.
Hapo jana usiku, moshi mweusi ulionekana ukifuka kutoka Vatican ishara
kwamba makadinali hawajaafikiana kuhusu ni nani atachukuwa wadhifa wa
Baba Mtakatifu. Mara baada ya kuafikiana kwa kupata thuluthi mbili ya
kura, moshi mweupe utaonekana na kengele za kanisa kuu la Mtakatifu
Petro kupigwa.
Hali ilikuwa kinyume na matarajio
Makadinali wakiwa katika misa maalum
Makadinali hao jana walifungiwa katika kanisa la Sisitine kwa
siku ya kwanza baada ya ibada na maombi ya kuwatayarisha kwa ajili ya
wajibu huo muhimu katika kanisa Katoliki. Jana usiku kura ilipigwa mara
moja na kama ilivyotarajiwa na wengi, makadinali hawakuafikiana.
Hakuna baraza la makadinali katika nyakati za sasa ambalo limemchagua
papa katika siku ya kwanza ya upigaji kura, kwa hivyo matokeo ya hapo
jana hayakupokelewa kwa mshangao. Kawaida awamu ya kwanza huchukuliwa
kama mchujo wa wanaopigiwa upatu.
Vatican imechukua hatua za tahadhari ili kusiwepo kwa mawasiliano ya
aina yoyote kati ya makadinali hao 115 na ulimwengu kuepusha ushawishi
wa nani atakayechaguliwa. Hakuna matumizi ya simu, redio, televisheni
wala mitandao.
Kashfa za kanisa katoliki
Kiongozi aliyejiuzulu Papa Benedict XVI
Papa mpya ataubeba mzigo uliomfanya Papa Benedict wa 16
kutangaza mwezi Februari kuwa umemuelemea. Kanisa Katoliki linazongwa na
kashfa chungu nzima za udhalilishaji watoto na visa vya kufichuka kwa
siri za makao makuu yake ya Vatican zinazodai kuwepo kwa ufisadi na
malumbano ya wenyewe kwa wenyewe.
Aidha linakumbwa na ushindani kutoka makanisa mengine katika udhibiti wa
wafuasi hasa barani Ulaya ambayo ni ngome yake. Inakisiwa kuwa kanisa
hilo lina waumini bilioni 1.2 kote duniani.
Wanaopigiwa upatu kutangazwa kuwa papa mtakatifu mpya ni Angelo Scola
kutoka Italia, Mbrazil Odilo Sherer ambaye akichaguliwa atakuwa papa wa
kwanza ambaye hatoki barani Ulaya tangu kuchaguliwa kwa Papa Gregory III
yapata miaka 1300 iliyopita.
No comments