Breaking News

Francis wa Kwanza: Papa mnyenyekevu bali mhafidhina

Kadinali Jorge Mario Bergoglio wa Argentina aliyechukua jina la upapa la "Francis wa Kwanza" ndiye Papa mpya wa Kanisa Katoliki lenye waumini wapatao bilioni 1.2 duniani kote na wa kwanza kutokea Amerika ya Kusini.
Sauti ni ya utulivu inayowasilisha ujumbe wa kimapinduzi."Cambia todo cambia" yaani yote yanabadilika ni maneno ya wimbo wa mwanamuziki maarufu sana katika Amerika ya Kusini, Mercedes Soza.
Katika wimbo wake mwimbaji huyo amezipanga beti zinazosema:
"Mchungaji na mifugo yake
Jua katika njia yake
Njia anayoelekea mhamiaji
Na kilichobadilika jana
Lazima kitabadilika tena hapo kesho."
Wimbo huo wa mwimbaji kutoka Argentina ni sehemu ya muziki katika filamu moja ya Kitaliano inayoitwa Habemus Papam, yaani "Tunaye Papa". Filamu hiyo ilitambulishwa kwenye tamasha la filamu la mjini Cannes , Ufaransa. Sasa filamu hiyo imethibiti kuwa hali halisi
Anatoka Amerika ya Kusini
Waumini wa Kikatoliki wakishangiria mjini Buenos Aires, Argentina, baada ya Francis I kutangazwa kuwa Papa.
Kuchaguliwa kwa Kadinali Jorge Mario Bergoglio kutoka Argentina maana yake ni kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya upapa, amechaguliwa mwakilishi wa Yesu Kristo anayetokea nje ya bara la Ulaya.
Baba Mtakatifu mpya, Francis wa Kwanza, anatofuatina na viongozi wengine wa Kanisa Katoliki kwa mambo mengi. Kama Askofu Mkuu wa Buenes Aires hakutaka kuishi kwenye kasri na wala hakutaka kuwa na dereva. Aliishi katika makaazi ya kawaida na alipanda basi kama watu wa kawaida.
Baba Mtakatifu huyo mpya mwenye umri wa miaka 76 alipenda kujipikia chakula chake mwenyewe. Sifa yake kama kiongozi mwenye unyenyekevu ilithibitika jana katika kauli zake za kwanza.
Alitokeza akiwa amevalia vazi jeupe la kipapa na mbele ya maelfu ya waumini waliokuwa wanashangilia kwenye uwanja wa Mtakatifu Petro, makao makuu ya Vatican, lakini badala ya kuwabariki watu kama ilivyo desturi, ni yeye Papa Francis aliyewaomba waumini wamsalie.
Shabiki wa kandanda lakini mhafidhina
Waumini wa Kikatoliki wakishangiria mjini Buenos Aires, Argentina, baada ya Francis I kutangazwa kuwa Papa.
Wazazi wa Papa Francis wenye nasaba ya Kitaliano, walihamia Argentina miaka kadhaa nyuma. Kiongozi huyo mpya wa Kanisa Katoliki anasemekana kuwa ni shabiki wa kandanda, muziki na ana sifa kubwa ya kuwa mtetezi wa masikini, na hivyo anatarajiwa kuzigusa nyoyo za watu kwa unyenyekevu wake.
Lakini pia, kama walivyo mapapa wengine waliotangulia, naye pia ni mhafidhina. Katika miaka ya nyuma aliwahi kukwaruzana na Rais Christina Kirchner wa Argentina juu ya masuala ya mashoga, pale mwaka 2010 alipoziita ndoa za jinsia moja kuwa ni njama za kuuteketeza mpango wa Mungu.
Pia Papa Francis wa Kwanza anapinga utoaji mimba na wanawake kuwa makasisi.
Lakini pia inapobidi anatofuataina na viongozi wenzake wa kidini. Amewahi kuwalaumu waziwazi baadhi ya viongozi hao kwa unafiki na waliosahanu kwamba Bwana Yesu aliwatibu wakoma na alikula chakula pamoja na makahaba.
Francis wa Kwanza ni Baba Mtakatifu wa 266 anayechukua nafasi ya Papa Benedikt wa 16 aliejiuzulu mwezi uliopita.

No comments